Kazi Wakati wa Ujauzito: Nini Ni Salama?
Imekaguliwa kitabibu na Midwife Rhoda James Kallabaka, 2026-09-16.
Wajawazito wengi Tanzania huendelea kufanya kazi mpaka karibu na muda wa kujifungua—ofisini, sokoni, saluni, dukani au shambani. Kwa mimba isiyo na complications, unaweza kuendelea kufanya kazi, lakini mwili unaweza kuhitaji mapumziko na marekebisho kadri mimba inavyokua.
Fahamu haki zako kazini
Kwa ajira rasmi Tanzania Bara, sheria inatoa angalau siku 84 za likizo ya uzazi yenye malipo, au siku 100 kwa aliyejifungua watoto zaidi ya mmoja. Baba pia ana angalau siku 3 za likizo yenye malipo.
Toa taarifa ya likizo mapema kwa mwajiri na ambatanisha uthibitisho wa kitabibu. Ujauzito haupaswi kuwa sababu ya kufukuzwa au kubaguliwa kazini. Kama huelewi masharti yako, zungumza na HR au ofisi ya kazi.
Kwa mama anayejiajiri, panga mapema mtu wa kusaidia biashara, muda wa kupumzika na akiba ya kipindi ambacho hutafanya kazi.
Rekebisha kazi kulingana na mwili wako
Kama unasimama muda mrefu, kaa kwa mapumziko mafupi, badilisha position na vaa viatu vyenye support nzuri.
Unapochukua kitu chini, pinda magoti badala ya mgongo. Epuka kubeba mzigo unaokufanya ukaze tumbo, ushindwe kupumua au upoteze balance.
Ukiwa kwenye jua au mazingira ya joto, kunywa maji mara kwa mara na pumzika sehemu yenye kivuli au hewa.
Ofisini, usikae kwenye position moja kwa muda mrefu. Inuka, tembea kidogo na tumia mto mdogo ku-support mgongo.
Safari za kwenda na kurudi kazini
Katika safari ndefu, nyoosha miguu na tembea kidogo pale inapowezekana. Ukiwa kwenye gari, mkanda wa chini ukae chini ya tumbo, juu ya mifupa ya nyonga, na wa juu upite katikati ya matiti na pembeni ya tumbo.
Dalili za kuacha kazi na kutafuta msaada
Acha kazi na tafuta huduma ya afya haraka ukipata:
Damu au maji kutoka ukeni
Maumivu makali ya tumbo au mikazo yenye mpangilio
Kichwa kikali pamoja na kuona ukungu
Kizunguzungu kikali, kuzimia au kushindwa kupumua
Kuvimba ghafla usoni au mikononi
Mtoto kucheza kidogo kuliko kawaida
Kama una wasiwasi, fuata kikagua dalili au wasiliana na kituo cha afya.
Lini upunguze au kuacha kazi?
Hakuna wiki moja inayofaa kila mjamzito. Inategemea afya yako, hatua ya mimba na aina ya kazi unayofanya.
Kama una pressure kubwa, upungufu mkubwa wa damu, ujauzito wa watoto wengi au complication nyingine, unaweza kuhitaji kupunguza kazi mapema kwa maelekezo ya mhudumu wa afya.
Kumbuka: Kupunguza kazi si udhaifu. Lengo ni kuendelea na majukumu yako kwa namna iliyo salama kwako na kwa mtoto.
Fanya leo: Chagua badiliko moja la kufanya kazini—kupata kiti, kuongeza mapumziko, kubeba mzigo mdogo, kuweka maji karibu au kuzungumza na mwajiri kuhusu likizo yako.