Mtoto Ana Joto? Jua cha Kufanya na Wakati wa Kuwahi Hospitali

Imekaguliwa kitabibu na Midwife Rhoda James Kallabaka.

Kanuni muhimu kabisa: mtoto chini ya miezi 3 akiwa na joto la 38°C au zaidi anahitaji kuangaliwa na mtaalamu haraka, hata kama anaonekana yuko sawa. Watoto wadogo wanaweza kuwa na maambukizi makubwa bila kuonyesha dalili nyingi mwanzoni.

Kwanza, pima joto

Kumgusa mtoto kunaweza kukupa hisia kwamba ana joto, lakini kipimajoto ndicho kinachokupa jibu la uhakika zaidi. Kiwango kinachotafsiriwa kama homa kinaweza kutegemea sehemu na njia iliyotumika kupima.

Muhimu si kuangalia namba pekee—angalia pia mtoto alivyo: anakunywa? anacheza au kuitika? anapumua vizuri? anakojoa kawaida?

Ukiwa nyumbani

Mpe mtoto maziwa na vinywaji vinavyofaa umri wake mara kwa mara ili asipungukiwe maji. Mvishe nguo nyepesi na usimfunike kupita kiasi.

Kama ana discomfort, paracetamol inaweza kutumika kwa kipimo sahihi kulingana na uzito na maelekezo ya mtaalamu—si kwa kubahatisha kijiko. Kwa mtoto chini ya miezi 3 mwenye homa, usicheleweshe kwenda kupata huduma kwa kujaribu dawa nyumbani kwanza.

Haya usifanye

Usitumie maji ya barafu, usimpake pombe/spiriti na usimpe aspirin. Pia si lazima kulazimisha joto lirudi kawaida kwa kila gharama; dawa za homa hutumika zaidi kumsaidia mtoto mwenye discomfort ajisikie vizuri.

Usisubiri nyumbani kama...

Pia tafuta ushauri wa mtaalamu ikiwa mtoto anaendelea kuonekana mgonjwa hata joto likishuka, hali yake inazidi kuwa mbaya, au homa inaendelea kwa siku kadhaa.

Baada ya kliniki

Mpe dawa kama alivyoelekezwa na usitumie dawa zilizobaki kutoka ugonjwa uliopita bila maelekezo mapya. Kama hali haiboreki au inazidi kuwa mbaya, mtoto anahitaji kuangaliwa tena.

Fanya leo: Kama nyumbani hakuna kipimajoto cha digital, ni kifaa kizuri kuwa nacho. Homa inapokuja, hutategemea kugusa paji la uso pekee—utakuwa na namba ya kuanzia.