Meno ya Mtoto Yanapoota:Dalili za Kawaida na za Tahadhari

Imekaguliwa kitabibu na Midwife Rhoda James Kallabaka.

Karibu kila usumbufu wa mtoto kipindi meno yanapoanza kuota huitwa “ni meno.” Lakini si kila dalili ni ya meno, na kudhani hivyo kunaweza kuchelewesha matibabu.

Meno huanza lini?

Kwa watoto wengi, jino la kwanza huonekana karibu miezi 6, mara nyingi likiwa la mbele chini. Wengine huanza mapema au baadaye, na hilo linaweza kuwa kawaida. Watoto wengi huwa na meno yote 20 ya utotoni kufikia karibu miaka 3.

Dalili za kawaida

Mtoto anaweza kuwa na udenda mwingi, kutaka kutafuna vitu, fizi kuwa nyeti au kuvimba kidogo na kukereka kiasi. Unaweza kumsaidia kwa kusugua fizi kwa kidole safi au kumpa teether/kitambaa safi kilichopozwa.

Hizi si dalili za meno

Homa ya 38°C au zaidi, kuhara, kutapika au mtoto kuonekana mgonjwa sana si dalili za kawaida za meno. Usisubiri “meno yapite”—mtoto anapaswa kuangaliwa ili kujua chanzo halisi.

Kuhusu “meno ya plastiki”

Kuna imani kwamba mtoto mwenye homa au kuhara ana “meno ya plastiki” yanayopaswa kuchanwa au kung'olewa. Usichane fizi wala kung'oa jino la mtoto. Vitendo vya aina hii vinaweza kusababisha kutokwa damu, maambukizi na madhara makubwa, huku ugonjwa uliomsumbua mtoto ukichelewa kutibiwa. Tanzania pia inatambua infant oral mutilation kama desturi hatarishi kwa afya ya watoto.

Mtoto akiwa na homa, kuhara, kutapika au anaonekana mgonjwa, mpeleke kituo cha afya.

Tunza jino la kwanza

Jino la kwanza likitokea, anza kulisafisha mara mbili kwa siku kwa mswaki laini na kiasi kidogo sana cha toothpaste yenye fluoride—kama punje ya mchele. Epuka kumlaza mtoto na chupa ya maziwa au kinywaji chenye sukari mdomoni.

Kumbuka: Meno yanaweza kumsumbua mtoto kidogo, lakini usiite kila ugonjwa “meno.”